KUPATA CHOCHOTE UNACHOKITAKA


Binadamu ni kiumbe pekee anayejikataa jinsi alivyo”. Haya ni maneno ya Albert Camus mtafiti wa tabia za binadamu na  mwanafalsafa maarufu. Msemo huu ni kweli kwani hakuna mtu anayeridhika tu na hali yake aliyonayo bali kila siku hutaka kufika hatua fulani katika nyanja zote au katika nyanja fulani fulani za maisha yake. Changamoto kubwa inakuja ni namna gani atakipata kile anachokitaka; hapa ndipo kila mtu hutoka kivyake na wengine hudhubutu hata kutumia njia haramu kitu ambacho sio kizuri hata kidogo. Wengine hufuata njia sahihi, hujibidiisha sana na hatimaye hupata kile wanachokitaka. Basi, naomba nichukue nafasi hii kukushirikisha njia mbili zitakazo kusaidia kupata chochote unachokitaka.

Njia ya kwanza; Saidia Wengine.

Unaweza kupata chochote unachokitaka katika maisha yako iwapo utawasaidia watu kupata wanachokitaka. Watu unaokutana nao kila mahali wanapesa nyingi sana za kwako ila wanasubiri tu uwasaidie kitu wanachokitaka kisha watakupa hizo pesa. Swali ni je, utawasaidia kitu gani? Ili mtu umsaidie ni lazima mtu huyo awe anahitaji kitu unachotakakumsaidia. Watu wote unaokutana nao wanamahitaji mbalimbali ambayo naweza kuyaweka katika makundi matano. Makundi hayo ni haya yafuatayo;-

Kundi la kwanza, UHAKIKA. Kila mtu anataka awe na uhakika wa kuishi, uhakika wa nyakati zijazo,uhakika wa mradi wake n.k. Kwahiyo kama utamsaidia aweze kuupata uhakika  huo lazima na wewe atakupa  unachokitaka. Jukumu ulilonalo ni kufikiria ni kitu gani utakifanya ili ukiwasaidia watu katika mambo yao wapate kuwa na uhakika katika mambo hayo wanayoyafanya.

Kundi la pili, FAIDA. Kila mtu anataka apate faida kwenye kila jambo analolifanya,mfano akiwa na biashara anataka apate faida kwenye biashara yake au kama yeye ni mkulima anataka apate faida kwenye kilimo chake au kama yeye ni msomi anataka apate faida kwenye elimu yake. Sasa iwapo utawasaidia watu wapate faida kwenye maisha yao uwe na uhakika utapata  unachokitaka.

Kundi la tatu, MAHUSIANO. Kila mtu anahitaji awe na mahusiano mazuri na mtu fulani au na watu fulani ili aweze kujisikia vizuri na ajione kama miongoni mwa watu  anaowapenda yeye. Kwahiyo kuwasaidia watu wapate hitaji hilo kwako ni njia nzuri sana ya kupata chochote unachokitaka.

Kundi la nne, KUKUA. Hakuna mtu asiyependa kukua katika elimu yake, uchumi wake, imani yake na katika mwili wake. Jitihada zozote za kuwasaidia watu wakue katika nyanja yoyote waliyonayo kwako ni mlango mkubwa sana wa kupatachochote unachokitaka.

Kundi la tano, KUCHANGIA. Nani katika dunia hii asiyependa kuchangia? Nani asiyependa mchango wake uonekane kwenye kizazi hiki au kizazi kijacho?. Kila mtu anapenda kuchangia katika hali na mali katika mambo mbalimbali, kinachokwamisha ni kukosa uwezo wa kuchangia. Wewe msomaji wa MORNING TANZANIA ukianza kuwasaidia watu wapate uwezo huo wa kuchangia katika mambo yao kwako ni mlango mkubwa sana wa kupata chochote unachokitaka.

Njia ya pili; Omba.

Unawezaje kupata unachokitaka kwa kutumia njia hii?
Kwa mujibu wa Tony Robbins katika kitabu chake “Unlimited Power” anasema ni rahisi mno kupata chochote unachokitaka kwa njia ya KUOMBA. Anaedelea kusema ni lazima uombe kwa bidii na utumie njia sahihi na kwa watu sahihi. Zifuatazo ni hatua za kupata unachokitaka wa njia ya kuomba.
1. Kifahamu unachotaka kukiomba.
Unapoomba kitu ni muhimu sana uwe dhahiri (specific), kwa sababu kutokuwa dhahiri kunaweza kupelekea unayemwomba akuone kama mbabaishaji. Jambo la muhimu ni lazima utaje unataka kwa kiwango gani, kiasi gani, unataka lini, wapi na kwa malengo gani. Lazima ukielezee kitu unachokitaka kwanza kwako mwenyewe na kwa yule unayemwomba. Katika hatua hii ni muhimu kumwambia unayemwomba namna utakavyo tumia kile atakachokupa. Lugha unayotumia kuomba ni muhimu sana, mfano unabiashara unaenda kwa mtu kuomba mkopo halafu unaandika barua unasema; Ninaomba fedha za kutosha kufungua tawi jipya la biashara yangu… . Uwe na uhakika kupata fedha ni vigumu lazima useme tafadhali naomba kiasi cha shilingi....

2.  Omba kwa mtu anayeweza kukusaidia.
Mara nyingi watu huomba kwa watu wasio sahihi na matokeo yake wanakosa wanachokitaka. Chukulia kwa mfano umekwazana na mpenzi wako halafu unaenda kuomba ushauri kwa mtu ambaye anamgogoro wa kimausiano na mpenzi wake unategemea kupata nini? Au unaenda kuomba ushauri kwa mtu asiyejua kutunza siri unategemea nini? Kwahiyo ili kupata unachokitaka ni lazima ujue mtu  sahihi wa kukusaidia unachokitaka.

3. Mwambie faida atakayoipata pale atakapokupa unachokitaka.
Mtu kukupa unachokitaka sio jambo rahisi. Watu wapo tayari kukupa unachokitaka pale tu watakapofahamu watakachokipata kutoka kwako baada ya kukupatia unachokitaka. Kwahiyo unapoomba kitu chochote kwa mtu yoyote kwanza mwambie atafaidika nini mara atakapokupa unachokitaka. Wale wanaoomba ajira wanalijua hili kwa undani.  Mfano umeenda kuomba pesa kwa mtu  unasema naomba unipe Shilingi 10,000/= ni vigumu sana kukupa lakini ukienda halafu ukamwambia naomba unikopeshe Shilingi 10,000/= halafu nitakurudishia shilingi 12,000/= baada ya mwezi mmoja. Ni rahisi zaidi mtu huyo kukupa hiyo fedha. Au unaomba ajira sehemu fulani labda wewe ni mtaalamu wa ramani lazima ujikite kumwambia unayemwomba namna utakavyomsaidia kwenye swala zima la ramani usitaje tu jumla jumla eti mimi nimesomea ramani najua kuchora vizuri najua hili na hili…n.k atakwambia sawa unajua hayo si ya kwako wewe mimi yananisaidia nini? Unaweza kukosa kazi. Unachotakiwa ni kumwambia ukiniajiri nitakuchorea ramani vizuri na nitazitunza kwenye mfumo wa softcopy ili iwe rahisi kufanya marekebisho pia ramani zote nitaziweka kwenye mfumo wa GIS ili ziweze kutumika katika kila sekta. Maelezo hayo ni kivutio na unaweza kupata kazi mapema.

4.  Omba kwa malengo na uwe na imani kwamba utapata.
Hapa unatakiwa uwe unajua kushawishi, lakini sio kushawishi kwa uongo lazima ushawishi katika kweli. Hatari ya kushawishi kwa kutumia uongo punde uongo wako utakapobainika kuwa ni uongo utajishushia hadhi na siku nyingine utakosa kupata unachokitaka. Kwenye kushawishi onyesha uwezo wako na uhakika wa kile unachokitaka, kama unaomba kazi onyesha kwamba unajua unachokiomba. Watu wengi sana wanauwezo mbalimbali lakini hakuna waombaji wanaoweza kushawishi wakapata vitu vile. Tahadhari usishawishi kwa malengo mabaya au mambo ya uovu.

5. Omba mpaka upate unachokitaka.
Hapa sina maana uombe kwa mtu mmoja tu mpaka akupe unachokitaka, bali omba kwa watu mbalimbali na kwa namna mbalimbali mpaka upate unachokitaka.
Mwanzoni mwa mwezi huu nilienda wilaya ya Meatu iko mkoa wa Simiyu nikakutana na rafiki yangu mmoja tukawa tunazungumzia somo hili akaanza kunambia kuna mkuu wake wa idara alikuwa na tabia ya kutuma maombi sehemu mbalimbali ya kutafuta ufadhili wa masomo yake ya uzamivu (masters). Alikuwa anatuma kwa zaidi ya miaka kumi na minane (18) lakini hakupata. Mwaka jana, 2014 habari njema ikamfikia amepata ufadhili na amechaguliwa kwenda Denmark kuchukua “masters” yake. Nini kilichomfanya apate alichokuwa anakitaka ni kuomba hadi apate alichokuwa anataka.

Kwahiyo mambo hayo mawili ukiyazingatia kwa makini ni njia mzuri sana ya kupata chochote unachokitaka.

Endelea kujua zaidi hapa hapa MORNING TANZANIA. Pia jiunge nasi bure kabisa kwa email ili tuwe tunakutumia makala moja kwa moja kwenye email yako punde makala inapotoka. Kujiunga nasi kwa email bonyeza maadishi haya na uandike email yako kwenye box iliyoko chini upande wa kulia. Au wasiliana nasi kwa email; morningtanzaniasite@gmail.com

MORNING TANZANIA, “power of minds”,
Hakuna kinachoshindikana.









0 maoni:

Chapisha Maoni